Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenye kufanya tendo zuri, akiwa ni mwanamume au ni mwanamke, na huku ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi tutampa maisha mema yenye utulivu duniani hata kama ni mchache wa mali, na tutawalipa huko Akhera thawabu zao kwa uzuri zaidi ya walivyofanya duniani} [An-Nahli: 97].
Na katika mambo ambayo huingiza furaha na ukunjufu wa moyo katika moyo wa muislamu ni mafungamano ya moja kwa moja na Mola wake bila kupitia kwa viumbe walio hai au waliokufa au, masanamu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu, ametaja katika kitabu chake kitukufu kuwa yeye yuko karibu na waja wake wakati wowote, anawasikia na anawajibu dua zao kama alivyosema kutakasika ni kwake: {Na watakapo kuuliza, ewe Nabii, waja Wangu kuhusu Mimi, «Mimi Niko karibu nao, Nasikia maombi ya muombaji yeyote anaponiomba. Basi, na wanitii Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka} [Al-Baqara:186].
Na ametuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kumuomba yeye, na akalifanya jambo hili la dua ni katika ibada kubwa ambazo hujikurubisha muislamu kwa Mola wake pale aliposema Mwenyezi Mungu: {Na amesema Mola wenu niombeni nikujibuni} [Ghaafir: 60]. Na Muislamu mwema daima huhitaji kwa Mola wake, na hudumisha dua mbele zake, na kujikurubisha kwake kwa kufanya ibada njema.
Na kwa hakika ametuweka Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu kwa hekima kubwa na wala hakutuumba kimchezo mchezo; na lengo ni kumuabudu yeye peke yake hana mshirika wake, na akatuwekea dini ya kimalezi iliyotimia na kuenea, hupangilia mambo yetu yote maalumu na yasiyokuwa maalumu, na imehifadhi sheria hii yenye uadilifu mambo ya dharura katika maisha, na mambo hayo ni: kuhifadhi Dini yetu, na nafsi, na heshima, na akili, na mali, na mwenye kuishi kwa kufuata maamrisho ya sheria na akawa ni mwenye kujiepusha na mambo ya haramu kwa hakika mtu huyo atakuwa kahifadhi dharura hizi, na ataishi kwa furaha na mwenye matumaini katika maisha yake bila shaka.
Na mafungamano ya muislamu kwa Mola wake ni yakina, yanapelekea katika nafsi utulivu na raha ya nafsi, na kuhisi utulivu amani na furaha, na kuhisi kuwa pamoja na Mola -kutakasika ni kwake- na kutilia kwake umuhimu na mapenzi yake kwa mja wake muumini, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu nikipenzi cha wale walioamini, huwatoa gizani na kuwaleta katika nuru} [Al-Baqara: 257].
Na mahusiano haya makubwa ni hali ya hisia zinazobebwa na kuneemeka kwa kumuabudu mwingi wa rehema, na kuwa na shauku ya kukutana naye na kuuchochea moyo wake kupaa katika anga ya furaha kwa kuhisi kwake utamu wa imani.
Na huo utamu ambao haiwezekani ujisifie wenyewe, isipokuwa mwenye kuonja kwa kufanya twaa na kujiepusha na makosa, ndiyo maana anasema Mtume-Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- “Amekwisha ionja ladha ya imani, yule mwenye kumridhia Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mola wake, na uislamu ndiyo dini, na Muhammad ni Mtume“.
Ndiyo ikiwa atahisi mwanadamu kila wakati yuko mbele ya muumba wake, na akamjua kwa majina yake na sifa zake zilizo nzuri, na akamuabudu kama vile anamuona, na akatakasa ibada yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na wala hakukusudia katika Ibada hiyo isipokuwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu -kutakasika ni kwake-, ataishi maisha mazuri yenye furaha katika dunia na mwisho mzuri huko akhera.
Hata matatizo ambayo yanamtokea muumini katika dunia, kwa hakika joto lake huondoka kwa baridi ya yakini, na kuridhia Qadari ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumshukuru yeye kwa Qadari zake kheri zake na shari zake na kuridhika kwa hayo yote kwa ukamilifu.
Na katika mambo ambayo anapaswa muislamu kuyapupia ili izidi furaha yake na utulivu wake, ni kuzidisha kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuisoma Qur’ani tukufu kama alivyosema Mtukufu: {Wale walioamini na zikatulia nyoyo zao kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, basi fahamuni vyema kwa kumtaja Mwenyezi Mungu nyoyo hutulia} [Al-Raad: 28].Na kila anavyozidi muislamu kumtaja kwake Mwenyezi Mungu na kusoma kwake Qur’an huzidisha mafungamano yake na Mwenyezi Mungu, na hutakasika nafsi yake na imani yake.
Na hivyo ndivyo inampasa muislamu kuwa na pupa ya kujifunza mambo ya dini yake kutoka katika vyanzo sahihi, ili amuabudu Mwenyezi Mungu kwa Elimu, kwa hakika amesema Mtume-Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-: “Kutafuta elimu ni lazima kwa kila muislamu“.
Na awe ni mwenye kujisalimisha na kufuata amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye amemuumba, sawa sawa amejua hekima ya kuumbwa au hakuijua, kwa hakika amesema Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu: {Na haipasi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke iwapo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wametoa uamuzi kwenda kinyume nao, kwa kuchagua lile ambalo si alilolihukumu kwao. Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, amekuwa mbali na njia ya sawa umbali ulio wazi} [Al-Ahzaab: 36].
Na rehema na amani za Allah ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na ali zake na Maswahaba zake.